logo

The Institute of Bible and Ministry

Enabling, mobilising and inspiring through life-long learning     

 

  

Bishop Charles Salalah 


 

Chair: Rev Falanta


 

Vice Chair: Prof Mgasa

Coordinator: Rev Tony & Cath Swanson


 

 Mrs Ruth Shija Mjumbe


Treasurer: Mrs Nhigula 
Mrs Mwakatobe 

Rev Batano Mratibu Msaidizi

KUJIKWAMUA KIUCHUMI MWENYEWE

Na

Prof. Magishi Nkwabi Mgasa

 

Katika Semina ya wainjilist Taasisi ya Biblia na Utumishi

Africa Inland Church (T) Dayosisi ya Pwani

2 Novemba 2007

 Maswali ya kujiuliza

  • Kwa nini uko hapa duniani?
  • Una malengo gani yako binafsi?
  • Je umeshafikia malengo yako yote?
  • Kwa nini hujayafikia?
  • Je umeridhika?
  • Kama hujaridhika unafanya nini ili ufikie malengo yako?
  • Je mambo gani yanayokuzuia au kukukatisha tamaa kufikia malengo yako?

Ninayo hakika wengi wenu mnayo majibu ya maswali haya. Napenda muwe wazi mbele za Mungu ili tuweze kuendelea na somo letu vizuri. Tumia kama dakika tano tu kujibu maswali haya muhimu ili kuwezesha kuendelea na somo letu vizuri.

Baada ya kujibu maswali haya basi kusanya karatasi yako na tuanze kusoma majibu ya kila mmmoja bila kutaja ni nani aliyeandika.


UTANGULIZI

Watu wengi wanaendesha maisha bila kuwa na uhakika wa kile wanachotaka kufanya au kwa kukata tamaa kabisa. Mara nyingi wanatazama mambo yasivyowezekana tu, wakijiona hawana uwezo, siyo wakamilifu, au hawana elimu ya kutosha. Kwa ujumla wanaishi kwa kujitetea kwa nini hawafanikiwi na kujijengea hoja za kuhalalisha jinsi gani wanavyoshindwa kufikia malengo yao au kufanikiwa. Wengine wamekwisha kuahirisha malengo yao mpaka hapo baadaye labda watakapopata elimu ya kutosha, watakapooa au kuolewa au watakapomaliza kusomesha watoto na pengine wengine mpaka watakapokuwa wchungaji au maaskofu.

Kosa kubwa watu wengi wanalolifanya ni kufikiria kuwa kuna mtu mwingine atakayekukwamua au atakayekuwezesha au aliyekukwamisha kufikia malengo yako na si wewe mwenyewe.

Ndiyo maana unaishi maisha ya kubabaisha (kubangaiza) huna mafanikio huna furaha ili mradi tu upo duniani unaishi kwa shida tu.

Napenda nikuambie kwamba ukweli usiopingika kwamba mtu pekee anayekukwamisha katika maisha yako ni wewe mwenyewe tu. Hakuna mwingine. Kama unataka ufanikiwe chukua hatua kumiliki maisha yako kwa asilimia mia (100%) wewe mwenyewe kwa kila jambo lolote utakalolipata maishani mwako.

Mawazo yetu na mwenendo wetu unatuangamiza na kuridhika na kuwa na maisha duni au kuwa na maisha ya wastani tu. Wengi wanasema  kuwa na mali au maisha ya juu ni dhambi kama andiko linavyosema kuwa huwezi kumtumikia Mungu na Mali (Andiko). Dhana hii lazima tuitafsiri vizuri kwani Mungu wetu hakutuumbia tuwe watu wa shida tu Mungu alituumba tumiliki vitu vyote vya dunia hii (Andiko).  Tunatakiwa tujiamini sisi sana na pia tumwamini Mungu sana

Lazima tuamini kutoka ndani ya moyo tunavyotaka maisha yetu yawe na ndivyo itakavyokuwa  kwetu ( andiko....). Kama mayoni mwako huamini utakuwa na maisha mazuri ni kweli huwezi kuwa nayo. Pingamizi kubwa iko ndani ya mawazo yako. Siyo kwamba Mungu amekupangia hivyo au Mungu kaishiwa  au wewe huna uwezo ila ni wewe mwenyewe umeshindwa kuona na kuamini mafanikio ndani ya moyo na mawazo yako. Mawazo yako ndiyo yamezuia baraka za Mungu ( andiko... Mawazo yangu niwawazieni ninyi ni ya mema siyo mabaya asema Bwana Mungu).

Kuna wengine wanafikiri na kujiridhisha kabisa kwamba hapo alipo ndipo kafikia mwisho wa uwezo na maisha yake ndiyo hayo na hawezi kufanikiwa hata afanye nini. Kama utaamini hivyo hujakosea ndivyo itakavyokua. Ndiyo maana ili kuishi maisha ya mafanikio na maendeleo ongeza wigo we maonao yako.


ONGEZA WIGO WA MAONO YAKO AU PANUA MAONO YAKO.

Ili kuishi maisha mazuri na ya kufurahisha anza kuwa na mtazamo wa kuamini kuwa itakuwa. Anza kujiona unafanikiwa katika kila lengo lako na amini hivyo kwa moyo wako wote na katika mawazo.

 Jipange kwa mafanikio na kweli utafanikiwa  Paulo katika waraka wake alimuombea Gayo sala hii ( 3 Yohana 1:1 ) mpenzi  naomba ufanikiwe  katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo. Mtume Paulo alijua kabisa kwamba kufanikiwa kunaanzia kwenye roho ya mtu. Yaani kuamini kwa moyo wako wote kuwa utafanikiwa ndipo yale unayoyaamini yanatokea. Lakini lazima uwe na maono na ujue unachokihitaji. Pia moyo wako wote uwe na uhakika na yale unayoyaamini. Kumbuka unapoamini kwa moyo wako wote nguvu za Mung ndipo zinapofanya kazi. Mungu huwasiliana moja kwa moja na roho. Chochote ukitakacho rohoni na kuomba toka rohoni Mungu anakipokea na kuandaa namna ya kukitekeleza. Roho yako ndiyo inakupa mawasiliano na Mungu. Ni kama vile SIM card kwenye simu zetu za mkononi. Kama namba ya rafiki yako ukiiweka kwenye SIM card ukibonyeza moja kwa moja utapata mawasiliano. Mungu wetu anawasiliana na sisi kupitia imani iliyo thabiti ndani ya roho zetu.

ONA MAFANIKIO YAKO MAWAZONI KWANZA

Bahati hutengenezwa kwenye mawazo na mawazo yakiingia rohoni. Hakuna mtu anayeweza kujenga nyumba bila kufikiri nyumba hiyo itakuwaje. Ndiyo maana kwanza lazima uchoreshe ramani na uone kwa uwazi jinsi itakavyokuwa na baadae ndipo utakapofanikisha. Akili yako ni kama Kompyuta na wewe ndiye mtaalamu wa kuiongoza. Ukiipa kompyuta  (akili yako) amri nzuri basi itafanya ilichoagizwa bila makosa.  Inabidi ukitaka mafanikiiyo uiambie kompyuta yako (akili yako) sawasawa nayo itafanya hivyo,   Kumbuka ukishaweka mawazo yako katika kufanikiwa na ukaamini moyoni mwako hivyo, bila shaka utafanikiwa. Pia utaona mambo mengi yanajitokeza kukuwezesha wewe ufanikishe malengo yako.

Unajua akili yako ni kama udongo. Udongo haujali umepanda mbegu gani. Udongo (akili yako) unastawisha chochote unachokipanda. Ukipanda mbegu mbaya utapata mimea mibaya, ukipanda nzuri utapata mimea mizuri. Kila upandacho (akilini) ndicho kitakachooota. Ukipanda mafanikio hakika utafanikiwa ukipandwa kushindwa hakika utashindwa.

TUMIA KILE ULICHO NACHO

Wakati mwingi watu wengi wanashindwa kuwa na mafanikio kutokana na kutojiamini au kutoamini uwezo wao. Pengine anajiangalia kielimu, kifedha, kimaumbile na mambo mengine mengi.  Katika hali hiyo badala ya kuangalia kile alichonacho ndicho kimsaidie anatafuta visingizio vya kuhalarisha kushindwa hata kabla hajafanya juhudi zozote. Mfano Musa alipokutana na Mungu pale kichakani. Kutoka 3:10-11  haya, basi,nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu wana wa Israeli, katika Misri. Musa akmwambia Mungu, mimi ni nani hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri?

Musa alikuwa namjua Farao vizuri sana na aliona mawazoni kwake kwamba kazi anayotumwa ni ngumu sana. Kwa mawazo yake aliona ni kazi isiyowezekana kabisa. Aliangalia ugumu wa Farao maana yeye alikulia kwake na anamfahamu vizuri sana . Moyoni mwake alikiri kushindwa na ndiyo maana akauliza "mimi ni nani" alijiona dhaifu wala hana uwezo wowote. Hivyo ndivyo watu wengi walivyo. Wanajitazama mapungufu waliyonayo, labda uwezo wa kifedha, wa kielimu, wa nguvu, wa afya na mambo mengi ya kujikatisha tamaa na kujiridhisha na hali waliyo nayo. Moja kwa moja wameshindwa kabla ya kuanza au kuchukua hatua yoyote. Mungu alizidi kumhakikishia uwezo wake na kwmaba atakuwa pamoja naye. Lakini tunaona Musa anazidi kukiri udhaifu. Kutoka  4:1 Musa akajibu, lakini Tazama hawataniamini, wala hawatasikia sauti yangu... hapa bado Musa anasimamia woga wa kibinadamu kuogopa kutenda jambo, hofu ni mbaya na wakati mwingi tunajitia hofu sisi wenyewe pamoja na kwamba Mungu amesema atatusaidia na atakuwa pamoja nasi lakini hofu inatawala.

Ni sawa na mtu anapowaza wazo labda la kuanzisha biashara. Moja kwa moja anaanza kuwaza mapungufu aliyo nayo. Labda fedha kidogo hii itawezaje kunifanikisha, labda wateja hawatapatikana, labda nitakula hasara, labda nitaibiwa, kwanza sina ujuzi na au sijasomea biashara na mabo mengine mengi tu ali mradi ahalalishe kukwama kwake. Kushindwa ku katika mawazo yetu tu ila Mungu anasema "Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe" Kutoka 3:12. Sasa Je kuna sababu yoyote ya kuogopa kufanya jambo lolote linaloweza kukuletea mafanikio au kukukwamua kiuchumi? Usitafute sababu za kujikwamisha mwenyewe angalia nini Mungu anachotaka ufanye na usonge mbele maana Mungu yuko pamoja nawe.

Mungu akamwabia Musa nini uliyonayo mkononi mwako? Akasema ni fimbo. Akamwambia itupe chini, nayo ikawa nyoka. Musa akakimbia mbele yake. Bwana akamwambia Musa, nyosha Mkono wako, kamshike mkia, (akaunyosha mkono wake akaushika mkia, naye akageuka kuwa fmbo mkononi mwake) Kutoka 4:2-4.

Unaona Mungu anavyomuuliza Musa nini uliyonayo mkononi mwako? Hili ni swali la kujiuliza kwa nini Mungu alimwuliza Musa hivyo?  Je wewe umewahi kujiuliza nini ulichonacho mikononi mwako? Maana kile ulicho nacho ndicho kitakachokuwezesha na Mungu akamdhihilishia Musa kwamba kile alichonacho kinaweza kugeuka kitu chochote kwa uwezo wa Mungu. Je wewe una nini mkononi mwako, weka chini, yaani kitumie kile ulichonach na utafanikiwa. Hapa sidhani kuna hata mmoja wenu anayeweza kusema kuwa hana kitu alichopewa na Mungu. Je kile ulichopewa na Mungu umekitumiaje? Usikishikilie tu na kuendelea kujidharau weak chini uone kitakavyokuletea mafanikio maana Bila shaka Mungu atakuwa pamoja nawe. Tafakali neno hili "Bila shaka" yaani kama huna shaka yaani uwe na imani moyoni mwako ndipo Mungu atakavyokuwa pamoja nawe. Mara nyingi watu wanashindwa kufanya jambo lolote nakile walicho nacho kwa sababu hawaamini moyoni mwao yaani wamejaa mashaka. Anaweza kuanzisha biashara lakini amejaa mashaka moyoni. Kwa namna hiyo Mungu hawezi kuwa pamoja nawe. Mungu alipenda kumuonyesha Musa kuwa kile alichanacha ndicho kitakachoweza kumsaidia na wote tunajua jinsi gani Musa alifanya miujiza mingi na fimbo yake baada ya kuwa na imani. Musa alikuwa mdhaifu kama mtu yeyote alivyo lakini baada ya kuamini alichokuwanacho alienda kwa Farao na kweli alishinda. Fimbo ya Musa iliwafanyia wana wa Israeli maajabu mengi makubwa na kuwaletea ukombozi kama vile Mungu alivyokusudia

Je wewe una nini mkononi mwako ambacho waweza kukitumia ili uweze kujikwamua kiuchumi? Tafakari mwenyewe na uone ni nini ulichonacho ambacho unaweza kukitumia uweze kufanikiwa.  Usijikwamishe mwenyewe kwa kudharau chochote ulichonacho kwani kama hutakuwa na shaka hakika utafanikiwa

USIWE NA MASHAKA NA UKIRI KILE UNACHOTAKA

Unafahamu unapokili udhaifu ndivyo inavyokuwa. Ukikiri ushindi pia unashinda na ukitaka mafanikio pia ukiri kufanikiwa. Ni vyema usiwe na shaka kabisa moyoni mwako kwa kile unachokitaka na ndipo utakapofanikiwa. Wakati mwingine ni vema hata ukaandika mahitaji yako na kuyaorodhesha vizuri kabisa ukawa unayasoma kila wakati ili moyo wako uyaweke na kuyaamini kwa dhati ni wazi utafanikiwa tu. Waweza hata ukawa unayatamka kwa kuyarudia rudia. Kile unachokitamka huwa. Ukitamka mafanikio utafanikiwa.

Hebu angalia mfano wa Daudi.  1Samwel 17:43-47 tafakari maneno aliyotamka Daudi wakati akipambana na Goliathi. "Bali mimi nakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya  Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuuwa mikononi mwangu, nami nitakupiga na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli"

Daudi amesimama kwa ujasiri kwa imani kukabili tatizo lililokuwa mbele yake kwa ujasiri. Yeye alijua hakika kwamba katika mapambano haya anaye Mungu. Ndiyo maana alisema minmi ninakujia kwa jina la BWANA wa Israeli. Hapo hakuangalia udhaifu wake. Aliangalia aliyenaye mbele yake ambaye ni mkuu kuliko shida yake. Je Daudi alikuwa na nini? Kwanza alikuwa mtoto tu! Pia hata silaha yake ilikuwa duni kabisa ukilinganisha na silaha za Goliathi. Tunaona (1 Samweli 17:49-54) Daudi akatia mkono wake mfukoni akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga mfilisti katika kipaji cha uso jiwe likamwingilia kipajini akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule mfilisti. Je Daudi yale aliyoyasema hayakutimia. Mungu akiwa upande wetu ni nani atakayetushinda? Na tunaona Daudi anasema wazi kuwa  "Ili dunia yote wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli" hapa yeye hakujitwalia utukufu wala yeye hakutaka kujulikana kuwa ndiye aliyefanya hayo. Hii inadhihilisha wazi imani aliyokuwa nayo moyoni hata kabla ya mapambano kuwa ni Mungu nidiye anampigania. Je wewe na mimi tunapoanza biashara au kitu chochote tunachokifanya tunayo imani kwamba tutafanikiwa na pia kwamba Mungu ndiye atatutendea na siyo akili zetu

Kila utakalolifanya tamka kwa imani na umtangulize Mungu utafanikiwa. Weka maono yako wazi kwa Mungu an uyatamke wazi jinsi unavyotaka iwe. Yaone mafanikio kama yolivyo moyoni mwako na uamini kuwa Mungu atatenda pamoja nawe na atekupa uwezo wa ajabu. Utashangaa jinsi Mungu atakavyokufanikisha. Daudi aliyaona yote yatakayotokea katika vita yake hata kabla hajaannza vita na kuamini kabisa moyoni bila shaka yoyote. Hakujali udhaifu aliokuwa nao au ukubwa wa Goliathi na silaha zake zenye nguvu wala hakutaka kukupotoshwa na kina Sauli katika nia yake.

Ukiangalia maandiko Sauli alijaribu kumpa mavazi na silaha. Tafakari sana Jambo hili, Sauli aliona huyu kijana hawezi kushinda na akaanza kumshawishi atumie vifaaa tofauti na alivyonavyo. Mimi natafsiri kwamba Sauli alikuwa anamwambia kwa vitendo kwamba wewe huwezi kushindana na Goliathi mpaka uwe na uwezo fulani kama kumkatisha tamaa. Haya ni mambo yanayojitokeza kila unapokuwa na nia ya kufanya jambo fulani watu wataanza kukukatisha tamaa. Na kuanza kukushauri kama alivyofanya Sauli kwa Daudi. Pengine wewe ungefanya hivi, au vile, au huna uwezo huu na ule au vyovyote vile ali mradi wakukatishe tamaa. Ndivyo ilivyo hata katika maisha. Wewe unaweza ukawa umefanya mipango yako yote vizuri kama Daudi lakini watu wanaweza kukukatisha tamaa kama utawasikiliza.

Daudi alisimamia azma yake na kuamini kile alichonacho ndicho kitakachomsaidia na wala hakuangalia watu wengine. Angalia tofauti kati ya watu wanaofanikiwa na wasiyo na mafanikiyo si kuwa na uwezo mkubwa ila ni ule uamuzi wao kutumia kile walicho nacho na uzoefu wao katika maisha.  Simama katika uwezo ulionao iwe kifedha, au kielimu,au kimaumbile au kiafya yote utayaweza ukiamini hivyo. Angalia Daudi alivyojibu „"siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu" (1 Samweli 17:39 (b). Hili jibu linatufundisha nini? Daudi aliamini kabisa uwezo wake pia uzoefu wake. Ingawa Sauli alidhani hana uwezo au uwezo wake ni mdogo yeye alikuwa na uhakika na uwezo wake na uzoefu wake. Usiogope maana Mungu atakibariki kile ulicho nacho na atakupa ushindi.

Hakika kile ulichonacho ndicho unaweza kufanya kazi nacho. Daudi aliridhika kabisa na hali yake na aliamini kwa hakika atashinda bila msaada wa kitu kingine chochote asichokijua. Unajua uwezo ulio nao Mungu atautumia huo huo kama utaamini kwa hakika moyoni mwako. Mungu ataandaa mazingira ya kukuwezesha na ataweka mipango yako vizuri kabisa ili ufanikiwe.

Wewe leo Je? Unaamini uwezo wako ni mkubwa kuliko tatizo ulilonalo? Maana yeye uliyenaye hashindwi lolote katika uso wa dunia hii.  Mungu anauliza (Yeremia 32:26-27). Tazama mimi ni BWANA Mungu wa wote wenye mwili Je kuna kuna neno gumu lolote nisiloliweza? Jibu  (Yeremia 33.3) Niite nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa magumu usiyoyajua. Je katika haja yako umemwita Mungu kwa imani au umetegemea akili zako mwenyewe.

OMBENI KWA IMANI MTAPEWA

Haja ya Moyo wako na ijulikane na Mungu. Wakati mwingine tunashindwa kumweleza Mungu vizuri yale tunayohitaji atutende. Hatuko wazi mbele za Mungu na hivyo tunashindwa kutimiziwa kama tunavyotaka. Ni vizuri unapokuwa na hitaji lako la mafanikio liweke vizuri na uwe na uhakika ni nini  unachataka na kwa nini. Malengo yako yowe yanaeleweka. (1 Samweli 1:10-14). Na huyo mwanamke alikuwa na uchungu moyoni mwake akamwomba BWANA akalia sana, akaweka nadhiri, akisema, ikiwa wewe utaniangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume,ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtotosiku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani mwake kamwe.

Hili ni ombi la Hanna na liko wazi na ukiendelea kusoma (1Samweli 1:13) basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake, midoma yake tu ilionekana kama ananena, sauti yake isisikiwe, kwa hiyo huyo Eli  alimdhania kuwa amelewa.Hapa tunajifunza nini? Hana ananena na moyo wake na anazungumza zungumza kuweka haja yake vizuri moyoni mwake na ndipo roho yake inawasiliana na Mungu moja kwa moja.

Pia tunaona anasema anachokitaka kwa uhakika. Mototo wa kiume, atamtoa amtumikie Mungu maisha yake yote. Mahitaji yake yanaeleweka vizuri anachokitaka na malengo yake vyote viko wazi. Watu wengi wanaendesha maisha bila malengo na mahitaji yao wenyewe hawayajui. Wanaomba Mungu kila wakati lakini hawasemi ni nini wanachotaka. Mfano ukiwa na mtoto anaomba umnunulie nguo labda ni mtoto wa kiume. Je utamnunulia nini? Unaweza ukamnunulia kaptula, au shati, au kanzu. Maana hajasema anahitaji nini. Halafu ukimpatia atasema mimi nilitaka suruali na koti zuri hii hainifai. Lakini angesema tangia mwanzo akataja kwa uhakika anataka nini na cha aina gani? Huoni kwamba ingekuwa rahisi sana kwa mzazi kumchukulia hicho kitu maana maelezo yanajitosheleza.

Hanna alipewa kama alivyoomba maana alikuwa wazi kabisa. Nakusaidia ndugu yangu ukihitaji labda kuwa na Gari weka mawazo yako wazi aina ya Gari, ukubwa wa gari na utaitumiaje. Pia ikiwezekana utafute hata picha yake uwe naye na ukae unaitazama tazam kila wakati ukisema maneno na kujihakikishia kwamba imekuwa yako. Rudiarudia maneno hayo asubuhi na jioni na ikiwezekana sema neno juu yahitaji lako kimoyomoyo au hata kwa sauti kama vile Hanna alivyokuwa akifanya. Kitendo cha namna hiii kinafanya moyo wako upokee maagizo hayo na yanakaa rohoni na ndipo kutakuwa na mawasiliano na Mungu. Ujue Mungu huwasiliana na Roho yako moja kwa moja. Ukishaweka wazi hitaji lako rohoni Mungu analipokea na kulifanyia kazi na mafanikio yanakuja. Hanna alifanya hivyo na ndiyo maana midomo yake ilionekana kuchezacheza natumaini alikuwa anarudiarudia maombi yake mpaka yazame vizuri rohoni ndipo Mungu akayapokea. 

CHUKUA HATUA

Kile tuanachofikiri au  tunachojua au tunachoamini hakina faida au hakiwezi kuleta matokeo yoyote kama hatuchukui hatua kukifanyia kazi. Ukumbuke matokeo yanatokana na kile tunachoamua kufanya.

Dunia haiwezi kukulipa kwa kile unachokijua, bali kwa kile unachofanya. Inashangaza sana kuwa watu wengi wanapoteza muda wao kupanga na kutafiti au kufikiri bila kufanya kitu chochote, lakini wanachohitaji hasa ni kuchukua hatua kuanza kufanya. Ukianza kufanya jambo unaamsha ari na uwezo mkubwa unaoweza kukuletea mafanikio.Kwanza unawafanya wale wanaokuzunguka kujua kwamba unayo nia ya dhati kutekeleza yale uliyoyaamua. Watu wanaamuka na kuanza kukuangalia kwa makini. Watu wenye malengo sawa na ya kwako wanaanza kujitokeza na kukushauri. Pia wewe mwenyewe unaanza kujifunza mambo kutokana na uzoefu na jinsi unavyoifanya kazi ambavyo usingeweza kujifunza kama ungeendelea kusikiliza na kusoma vitabu tu bila matendo. Utaanza pia kujua namna unavyoweza kufanya vizuri zaidi maana tayari umeshaanza. Mambo ambayo yalikuwa hayawezekani sasa yanaanza kuonekana ni rahisi na pia unagundua mbinu za kuifanya kazi vizuri zaidi. Pia utaanza hata kuvutia watu kukusaidia hata kukutia moyo. Kila kiti kinaanza kuonekana vizuri na mambo mazuri yanajitokeza mara tu utakapoanza.

Kuna jambo moja tu linalowatofautisha watu wenye mafanikio na wasio na mafanikio ni kwamba watu wenye mafanikio huwa wanachukua hatua ya kuanza au kutenda jambo badala ya kufikiri fikiri na kupanga na kupangua. Mara wanapokuwa wameandaa mipango yao, huanza mara moja kutekeleza azma yao. Hata kama hawajaanza vizuri wanajifunza kutokana na makosa wakati wanaendelea kuifanya hiyo kazi. Niliwahi kumshauri rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa amekata tamaa kabisa ya kujenga nyumba. Kila akiangalia uwezo wake ni mdogo, kipato chake hakitoshi kabisa basi anafika mahali anasema mimi haiwezekani kabisa kujenga. Kwanza vifaa vya ujenzi ni ghali sana na pesa alikuwa hana za kutosha. Nilipojaribu kumuuliza je una kiwanja? Akasema kiwanja anacho alikuwa amepewa zamani sana na kutokana na kutojiweza alikuwa anafikiri hata akiuze tu maana mwisho kinaweza kuvamiwa na watu. Aliponiambia ana kiwanja nilifurahi na kumwambia mbona kazi kubwa tayari imekwisha. Maana kupata kiwanja ni hatua kubwa sana katika ujenzi. Sasa nakushauri wewe anza mara moja kujenga usiubiri upate fedha za kutosha ndipo uanze. Hata kama utapata fedha ya kununua mchanga tu fanya hivyo na baadaye utakuwa unanunua polopole mpaka utafanikiwa. Utashangaa jinsi Mungu atakavyokusaidia mara tu utakapokuwa umeanzisha ujenzi. Utaona hata watu watapatikana kukusaidia katika njia mbalimbali hata mawazo tu. Yule rafiki yangu alitulia na kunisikiliza na nikaona tayari amekwisha kuamini hivyo akaanza kazi ya ujenzi kama nilivyomshauri. Leo hii yuko katika nyumba yake amekwisha kuikamilisha na hata umeme ameweka. Jambo ambalo kwa akili yake alikuwa analiona haliwezekani kabisa. Nilipokutana naye akanishuhudia jinsi Mungu alivyomsaidia yaani alipoanza tu, akawa anapata misaada toka kwa marafiki na watu mbalimbali ambao Mungu aliwapanga na hatimaye akakamilisha ujenzi huo.

Mwalimu mmoja wa saikologia ya uwezeshaji alifanya jaribio hili.  Alichuka noti shilingi 10000 na akawauliza wanafunzi wake"nani anataka kuchukua hii shillingi elfu kumi?".Watu wengi katika darasa hilo walinyosha mikono yao kuonyesha kuwa wanaihitaji hiyo noti. Wengine walinyosha kwa bidii sana na hata wengine kupiga kelele nipe mimi nipe mimi na kadhalika il mradi wasikike na kuonekana kuwa wanayonia ya kuichukua hiyo noti. Yeye aliendelea tu kusimama mbele ya darasa huku ameishikilia mkononi hiyo noti na hatimaye mtu mmoja aliinuka kwenye kiti chake na akajitokeza mbele kwa haraka sana na kuichukua hiyo noti toka mkononi kwake na akarudi kuketi kwenye kiti chake. Baada ya huyo mwanfunzi kuketi akiwa amejipatia shilingi 10000 kwa juhudi zake Mwalimu aliuliza kundi la wanafunzi hao. Mtu huyu amefanya kitu gani ambacho wengine wote humu darasani hamkukifanya? Ameamua kusimama na kuchukua hatua ya kuchukua hiyo noti toka mkononi kwangu. Amefanya kile kilichotakiwa kufanywa ili kuipata hiyo pesa toka mikononi mwangu. Na hicho ndicho unachotakiwa kufanya ili kufanikiwa maishani. Lazima uchukue hatua za makusudi kufuatilia na kuchukua. Kadiri unavyofanya haraka kutekeleza jambo ndivyo utakapofanikiwa. Je wangapi katika darasa hilo walikuwa wanaitaka hiyo noti na wakajizuia wenyewe?  Nafikiri wengi walijizuia wenywe kwa visingizio mbalimbali na mwalimu alipowauliza walikuwa na majibu mengi kama:

          „"Sikutaka kuonekana ni mhitaji wa hiyo pesa"

          „"Sikuwa na uhakika kama kweli utaitoa hiyo noti"

          „"Nilikuwa mbali sana nisingeweza kuwahi"

          „"Nilidhani watu wengine wanaihitaji zaidi kuliko mimi"

          „"Sikutaka kuonekana nina uchu wa pesa"

          „" Niliogopa nisiwe nafanya makosa na watu wangenielewa vibaya"

          „"Nilikuwa nasubiri maelekezo zaidi"

haya ndiyo mawazo na mengine mengi yanayoweza kumkwamisha mtu kufanikiwa katika lolote lile. Ukweli ni kwamba unapokuwa na wasiwasi ndivyo unavyoshindwa kufanikiwa katika lolote. Ukiogopa huwezi kufanya lolote lazima utambue udhaifu huo na uuvunje kwa nguvu za Mungu. Kataa kuwa mwoga kwani woga pia ni dhambi. Muombe Mungu akuondolee woga huo na uthubutu kuanza kutekeleza malengo yako uliyonayo

FANYA  KAZI  NDIPO UTAKAPOFANIKIWA

2 Wafalme 4:1-7.

Basi mwanamke mmoja miongoni mwa manabii alimlilia Elisha, akasema , Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa anamcha Bwana;na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. Elisha akamwambia nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu, wala usitake vichache. Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vyote navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe;hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina . Ikawa vilipokwisha kujaa vile vyombo,akamwabia mwanawe niletee tena chombo. Akamwambia hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema,  Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako;nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.

Katika somo hili tunaona mwanamke mjane analalamika kwa Elisha akionyesha jinsi gani ana shida kwani anadaiwa. Ukisoma mistari hii pengine mama huyu alitegemea kuwa Elisha angempatia fedha ili aweze kutimiza haja yake. Lakini badala yake Elisha anamuuliza yeye ana kitu gni nyumbani. Mama huyu anasema hana kitu chochote ila chupa ya mafuta.

Ni wazi kwamba usemi huu ni wa kukata tamaa kabisa na kuona kwamba uwezo wake ni mdogo sana na hata alichonajo hakiwezi kumsaidia lolote. Cha kushangaza Elisha anamwambia akakusanye vyombo amiminie mafuta hayo katika vyombo. Tena anamwambia akakusanye vyombo vingi na siyo vichache.  Je  wewe ungefikirije? Kwa nini Elisha anafanya hivyo? Kwa nini Elisha asitoe pesa mara moja na badala yake anahitaji yule mama ajishughulishe kufanya kazi ya kutafuta vyombo ili avijaze mafuta?

Ni wazi kwamba andiko hili linaonyesha jinsi Mungu anavyotaka tufanye. Kwanza ana hitaji tuwe na imani na uwezo tulio nao naye katika uwezo huo atatubariki. Yaani kile ulichonacho Mungu atakibariki na kukifanya kizae sana ili mradi tu imani yetu ni kubwa juu ya kile tulichonacho.  Tena Elisha anamwambia mama huyu asikusanye vyombo vichache akusanye vingi. Mungu ana uwezo wa kujaza vyombo vyetu vyote tulivyo na uwezo kuvitafuta. Yaani baraka za Mungu siyo chache ni nyingi sana.

Mama huyu alidharau sana kile alichokuwa nacho lakini kitu kikubwa alichokuwa nacho ni kuamini ushauri aliopewa na Elisha na akatekeleza bila kuhoji maswali. Tunaona Elisha alimhitaji mwanamke huyu ashiriki kikamilifu yeye na wanae ili wapate vyombo wajaze mafuta. Kwa hiyo Mungu anatutaka tufanye kazi kwa bidii sisi na familia zetu kwa ushirikiano. Kila mmoja kwa nafasi yake. Kwa akili ya kibinadamu bila imani jambo hili aliloagiza Elisha lilikuwa gumu kwani ingekuwa vigumu kuamini kwamba haya yanaweza kuwezekana. Lakini mama huyu anaamini moja kwa moja na anafanya livyoagizwa.

Jambo hili linadhihilisha wazi kuwa ukiamini  yawezekana kabisa. Ule uwezo wako mdogo pamoja na imani iliyo kuu Mungu anaweza kukufanyia maajabu makubwa kama alivyofanya kwa huyu mama. Ni wazi Mungu atakujaza na kufurika kama jinsi alivyofanyiwa huyu mama.

Baada ya vyombo kujaa bado Elisha anamuagiza mama huyu aende akayauze mafuta hayo iliapate pesa. Hapa ni wazi kwamba ili upate pesa lazima ufanye kazi. Kazi  ya kuuza mafuta haya katika vyombo hivi vyote ni ngumu na siyo rahisi. Watu wengi wanataka mafanikio yaliyo rahisi bila jasho.Hilo jambo halipo na ndiyo maana  Elisha anazidi kumpa kazi huyu mama ya kuuza mafuta hayo. Mama huyu bado anavumilia na kuendelea na kazi ya kuuza hayo mafuta. Bila shaka alifanikiwa na deni lake alilipa na pia akabakiwa na ziada ya kutuma yeye na wanae.

Andiko hili linadhihilisha wazi ni lazima kujituma na kuwa na bidii na uvumilivu sana. Maana mafanikio yanaweza kuwa siyo ya haraka inabidi upitie hatua mbalimbali hadi kufikia mafanikio. Unajua watu wengi wanapookoka wanafikiri kuwa kufanya biashara ni dhambi. Je Elisha alipomuagiza huyu mama akauze mafuta. Je hiyo haikuwa  biashara? Kufanya biashara ni njia mojawapo ya kuweza kujikwamua kiuchumi. Mtaji wa kuanzisha biashara siyo lazima uwe mkubwa. Mtaji wako mdogo utakaoweza kuupata basi huo huo utumie vizuri na unaweza kufanikiwa.

Angalie usikalie uwezo wako na kudai ni mdogo. Angalia wale watu waliopewa talanta (ANDIKO). Yule aliyefanya biashara na kuzalisha aliongezewa na nyingine tajiri alipokuja. Lakini yule aliyekalia kulalamika na kusema kusema ni kidogo na anaogopa mwenye mali akaichimbia bila kuzalisha alinyang'anywa na kile alichokuwa nacho. Mungu wetu anachukizwa sana na watu wanaokalia vipawa bila kuvifanyia kazi. Angalia usije ukanyang'anywa hata hicho ulichonacho.

Mara nyingine tunatafsiri maandiko vibaya na kuhalalisha mambo yanayoweza kutudidimiza katika dimbwi la umasikini. Mfano (ANDIKO) wengi huwa wanadhani andiko hili lianasema tuishi bila kazi kama ndege wa angani kwani wao hawavuni wala hawalimi lakini wanakula. Hebu tafakari maisha ya Ndege, ni kweli kwamba ndege hana shamba. Je ndege akilala kwenye kiota Mungu atamletea chakula humo. Ndege kwanza ni mnyama mwenye bidii sana ya kazi. Anaamka mapema asubuhi kwenda kutafuta chakula. Asipotoka kwenye kiota hawezi kuona hata mtama uliomwagwa kwenye mashamba. Ni kweli kwamba hakuulima lakini inabidi awe na juhudi ya kuutafuta na kuupata ulipo. Pia anabeba hata kupelekea watoto kwenye kiota. Hii yote ni kazi anayofanya ndege ili kuweza kufanikiwa. Je wewe mwanadamu ni haki kweli ukae tu bila kazi. Vitu vyote vya dunia hii Mungu amempa mwanadamu avitumie kila kitu Mungu ametuandalia. Sisi tunachotakiwa kufanya ni kuvitafuta na kuvikusanya kama ndege wanavyofanya.

        

'It was He who gave some to be apostles, some to be prophets, some to be evangelists, and some to be pastors and teachers, to prepare God's people for works of service, so that the body of Christ may be built up until we all reach unity in the faith and in the knowledge of the Son of God and become mature, attaining to the whole measure of the fullness of Christ.'  

 Ephesians 4:11-13


        Mt Kilimanjaro


 

      Lake Victoria

 

 

Tanzania village

 

Woman - Mwanamke

 


Swahili proverbs:

Liandikwalo halifutiki - 

What is written by God cannot be rubbed away. 

 

 Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo - 

As you bring up a child so he will grow.

 

The Institute of Bible and Ministry: Enabling, mobilising and inspiring through life-long learning.

Address: AICT Coastal Diocese, PO Box 6753, Madaraka, Morogoro, Tanzania

Email: instituteofbibleandministry@gmail.com

  Facebook logo

Our website uses cookies so that we can provide a better service. Continue to use the site as normal if you're happy with this, or find out how to manage cookies. close [x]